Obama hatimaye ajiunga na Facebook
- Saa 5 zilizopita Mshirikishe mwenzako
Rais wa Marekani Barack Obama hatimaye amejiunga na Facebook, na ujumbe wake wa kwanza umekuwa ni wa kuhimiza watu kuchukua hatua kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ikulu ya White House kwenye ukurasa huo wake imepakia video ya Obama akitembea katika eneo la South Lawn katika ikulu ya White House.
Hatua yake ya kujiunga na Facebook, mtandao wa kijamii wenye zaidi ya watumiaji bilioni moja, inaonekana kama juhudi za kiongozi huyo kuwafikia zaidi vijana na makundi mbalimbali ya watu.
“Natumai mtachukulia huu kuwa ukumbi ambao tunaweza kutumia kujadiliana kuhusu masuala muhimu kuhusu taifa letu,” anasema kwenye video hiyo.
Obama anaonekana akitembea kwenye bustani hiyo ambayo imekuwa chini yake kwa miaka saba iliyopita, ambayo kama anavyosimulia, ina mbweha, mwewe na vichakuro.
Lengo kuu la kisiasa hata hivyo linaonekana kuhimiza ulimwengu kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Obama atazuru Paris mwezi Desemba, kutafuta uungwaji mkono wa mkataba wa kuweka vikwazo kwa mataifa kuhusu viwango vya utoaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani.
Kutokana na hali kwamba Bunge la Congress linadhibitiwa na chama cha Republican, ambacho hakijatambua hatari inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi, anahitaji kutafuta uungwaji mkono zaidi hata nyumbani.
White House imesema inatumai Facebook itasaidia kama ukumbi wa kubadilishana mawazo.
“Ukurasa huu utawapa Wamarekani jukwaa la kubadilishana mawazo yao na Rais kuhusu masuala ambayo wanayajali sana,” amesema naibu mkurugenzi wa mkakati wa dijitali katika White House Kori Schulman.
Bw Obama alijiunga na mtandao wa kijamii wa Twitter mwezi Mei mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni