Breaking News

Jumapili, 15 Novemba 2015

Tujikumbushe uzembe wa mabeki wa Stars

Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars jana ilishindwa kutumia uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya mbao 2-2 dhiti ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tanzania ambayo ilianza kusaka ushindi kwa nguvu zote ilishindwa kutumia nafasi za wazi zaidi ya 15 baada ya washambuliaji wake Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu ,Elias Maguli kukosa umakini katika lango la wapinzani.

Hata hivyo goli la dk 40 lilofungwa na maguli na dk 60 iliyofungwa na Samatta ilitosha kuifanya timu hiyo kutawala mpira, kabla ya makosa ya mabeki kuruhusu magoli 2 ndani ya dk 5, na kuifanya Algeria kusawazisha mabao yote na kubali ubao wa matangazo kuwa 2-2.

Alhamisi, 12 Novemba 2015

Kimenuka Simba,Matola abwaga manyanga

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
KOCHA Msaidizi wa Simba SC, Suleiman Abdallah Matola amejiuzulu nafasi hiyo kutokana na kile alichodai kutolelewana na Kocha Mkuu, Muingereza, Dylan Kerr.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE usiku huu, Matola amesema kwamba amefikia uamuzi huo baada ya kuona maelewano na bosi wake huyo yanazidi kuwa magumu kila kukicha.
“Ni jambo la muda mrefu, huyu kocha hasikilizi ushauri wangu, imefikia sasa ananichukia na kazi haziendi tena. Sasa nimeona ili kuepusha matatizo zaidi, nimuachie yeye timu,”amesema Matola.
Matola amesema kwamba haoni mwelekeo wowote mzuri kwa Simba SC chini ya kocha huyu Muingereza ambaye hasikilizi ushauri, ndiyo maana ameamua kujitoa.
Suleiman Matola (kulia) ameachia ngazi Simba SC baada ya kutofautiana na bosi wake, Dylan Kerr (kushoto)

“Nimekutana na uongozi, nimewaambia juu ya uamuzi wangu, wakanisihi sana nisifanye hivyo, lakini nikashikilia msimamo wangu. Wakaniambia hata nirudi kufanya kazi timu za vijana, lakini nikawaambia nitajifikiria kwanza,”amesema Matola. 
Juhudi za kumpata Kerr kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa na hakuna kiongozi wa Simba SC aliyepatikana mapema jioni hii kuelezea sakata hilo.
Historia ya Matola ndani ya Simba SC inaanzia mwaka 2000 alipojiunga nayo kama mchezaji akitokea Kagera Stars (sasa Kagera Sugar) na aliichezea timu hiyo hadi mwaka 2005 alipohamia Super Sport United ya Afrika Kusini.
Matola alirejea Simba SC mwaka 2007 na kucheza kwa msimu mmoja kabla ya kustaafu moja kwa moja.
Kuanzia mwaka 2010 amekuwa kocha wa timu za vijana za Simba SC ambako baada ya kufanya vizuri akapandishwa kuwa Kocha Msaidizi, akianza kufanya kazi na Mcroatia Zdravko Logarusic, baadaye Mzambia, Patrick Phiri, Mserbia, Goran Koponovic na huyu wa sasa Kerr.
Haijawahi kutokea Matola akatofautiana na kocha yeyote kati aliyofanya nao kazi awali – na Muingereza huyu anakuwa wa kwanza kutofautiana na Nahodha wa zamani wa Simba SC.     

Jumatano, 11 Novemba 2015

Kansiime ndani ya Kigali Rwanda

Kama ilivyo kwaida ya tovuti ya Habarimpya.com kukujali wewe msomaji wake, ratiba ya tovuti yetu kwa sasa ni kukupatia burudani.
Bila shaka utakuwa umewahi kumsikia ama kumtizama mchekeshaji mweye vituko kila kukicha nchini Uganda, Anne Kansiime, na kama haujawai basi huu ni wakati wako mwafaka wa kuburudika na vituko vyake. hiii ndiyo kazi yake mpya akiwa Mjini Kigali nchini RwandA. June mwaka 2015.

Kazi imeanza Muhimbili

Siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kufanya ziara ya kushtukiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, hali imebadilika ghafla ambapo huduma za matibabu zimeanza kutolewa haraka na kwa ufanisi.
 
Aidha, uongozi wa hospitali hiyo umeanza kufanya mazungumzo na kampuni ya Philips kutengeneza mashine mbili za CT-Scan na MRI za vipimo mbalimbali vya magonjwa.
 
Juzi, Rais Dk. Magufuli alivamia ghafla hospitalini hapo kisha kumuondoa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Hussein Kidanto pamoja na kuivunja Bodi ya Hospitali baada ya kutoridhishwa na utendaji wao wa kazi.
 
Nafasi yake imechukuliwa na Profesa Lawrance Mseru, ambaye alianza kazi hiyo jana saa 4:00 kwa kufanya vikao na Menejimenti na Kamati Tendaji ya Hospitali.

                                             KUANZA KUKARABATI MASHINE
Akizungumza na Nipashe, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema uongozi wa hospitali hiyo umeanza kufanya mazungunzo na kampuni ya Philips kwa ajili ya kutengeneza mashine zilizoharibika. Alisema kazi hiyo itafanyika hivi karibuni baada ya wataalam wa kampuni hiyo kuwasili kwa kazi hiyo.
 
Alisema wana matumaini ya mashine hizo kufanya kazi kwa muda waliopewa na Rais Magufuli. “Tutakamilisha kazi hii ndani ya kipindi tulichopewa, tunachofanya sasa ni kuzungumza na kampuni husika waje kuzitengeneza ili tuanze kutoa huduma haraka kwa wagonjwa,” alisema Aligaesha.
 
PROFESA MSERU AANZA KAZI
Akizungumzia Mkurugenzi mpya, Aligaesha alisema kwamba Profeza Mseru aliripoti jana saa 4:00 asubuhi na kuitisha vikao mbalimbali kwa ajili ya kujua utendaji kazi wa hospitali hiyo. Alisema baada ya kukamilisha kazi ya kukutana na makundi mbalimbali ya wafanyakazi, atazungumza na vyombo vya habari kuelezea kazi yake hiyo mpya.
 
HALI ILIVYO SASA
Gazeti hili liliwashuhudia madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa hospitali hiyo wakifanya kazi kwa kasi tofauti na siku za nyuma. Wodi nyingi zilionekana kuwa na madaktari muda wote, kitu ambacho wagonjwa walieleza kwamba kimewafurahisha.
 
Hata hivyo, katika daftari la mahudhurio, imeelezwa madaktari bingwa kwa mara ya kwanza wamejihorodhesha mapema asubuhi. “Ninachokuambia leo ni mchakamchaka kila mtu anawajibika, kwa mara ya kwanza madaktari bingwa wamesaini daftari la maudhurio,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
 
AGIZO LA MAGUFULI LATEKELEZWA
Mgonjwa Chacha Makange, ambaye Rais Magufuli aliagiza apatiwe matibabu pamoja na vipimo, alisema ndani ya dakika sita zimebadilisha maisha yake na wagonjwa wengine.
 
Chacha ambaye anafahamika kutokana na kuishi ndani ya handaki kwa miaka mitano maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema jana alipatiwa vipimo katika kituo binafsi cha kupimia magonjwa cha Besta kilichopo Kinondoni jijini Dar es Salaam. Alisema anamshukuru Mungu kumkutanisha na Rais Magufuli na kusababisha maisha yake kubadilika ghafla.
 
Chacha alisema alipomuona Dk. Magufuli, alimuomba aongee naye dakika tano, lakini Rais alimpa dakika moja ya kuzungumza. Hata hivyo, baada ya kuguswa na matatizo yake, kiongozi huyo alimuongezea dakika nyingine tano na kuwa sita ambazo hatimaye zilibadilisha mfumo mzima wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
 
“Nilipoanza kuongea, Rais aliguswa, aliniangalia na kuniambia niendelee, nilitumia dakika sita kueleza matatizo yetu, namshukuru Mungu amepanga haya yote yatokee kwa ajili ya Watanzania,” alisema Chacha. Aliomba jamii ishirikiane katika kufarijiana na kusema bila hiyo hakuna upendo wa kweli.
 
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dk. Othman Kiloloma, alisema mgonjwa huyo amefanyiwa vipimo vyote na kitu kilichobaki ni kuvisoma na kumpatia tiba sahihi.
 Alisema Chacha anasumbuliwa na matatizo ya mgongo, hivyo matibabu yake yananahitaji umakini na muda mrefu.
 
“Tumetekeleza agizo la Rais, leo (jana) tulimpeleka mgonjwa katika vipimo vyote, tunachoangalia hapa ni kufanya matibabu yake yanayoendana na matatizo aliyokuwa nayo,” alisema Dk. Kaloloma.
 Akizungumzia tatizo la wagonjwa kulala chini, Dk. Kaloloma alisema litaondoka baada ya kufunguliwa kwa jengo jipya kutokana na wodi zilizopo kutohimili idadi kubwa ya watu wanaohitaji kupata huduma.
 
 NIPASHE

Mkenya alihusika kampeni za Lowassa

JESHI la Polisi Jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Idara ya ya Uhamiaji inaendelea kumchunguza mtu aliyekamatwa na hati za uraia wa nchi mbili, anayedaiwa kuwa mwanaharakati wa siasa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Anaandika Faki Sosi … (endelea).
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema mtu huyo aliyetambulika kwa jina la Bashiri Fenele Awale Ally, amekamatwa kutokana na utata wa uraia wake na jinsi ambavyo alivyokuwa akijihusisha na masuala ya siasa nchi Tanzania.
Kamanda Kova amesama kuwa mtuhumiwa huyo mwenye hati ya kuzaliwa ya Tanzania yenye namba D063711 kwa jina la Bashiri Abdi Ally ambapo ilionyesha kuwa amezaliwa Julai 11, 1969 katika hospitali ya Dodoma.
Lakini pia mtuhumiwa huyo amekamatwa na pasi ya kusafiria ya Kenya yenye namba C000529 ambapo ilionyesha kuwa alizaliwa Nairobi Kenya Julai 11, 1969 kwa jina la Bashir Fenal Abdi Ally Awadhi.
“Kwa uchunguzi wa awali pamoja na kumbukumbu zenye utata mtuhumiwa mtajwa sio raia wa Tanzania bali ni raia wa Kenya ambaye alipeleka maombi idara ya uhamiaji lakini bado hajakubaliwa,” amesema Kamanda Kova.
Wakati huohuo, Kamanda Kova amesema jeshi hilo limekamata waharifu saba wakiwa bunduki aina ya SMG moja, bastola sita na bunduki aina ya Mark 4 Riffle moja na risasi 62.
Kamanda Kova amesema waharifu hao ambao wana viashiria vya ugaidi walipanga kuvamia vituo vya polisi lakini kabla hawajatekeleza mipango yao wamekamatwa.
Kova amesema kuwa mpaka sasa jumla ya majambazi wanahusishwa na ugaidi wamefikia 74, wamekamatwa ikiwa pamoja na silaha 51 na risasi 890 za silaha mbalimbali.

Msaidizi wa Lowassa Mbaroni

Mwanamkakati wa aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bashir Awale, amekamatwa na kuwekwa ndani katika Kituo cha Polisi cha Kati.
 
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya timu ya kampeni ya mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, zinasema kuwa Awale alikamatwa juzi jioni kwenye maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam.
 
Taarifa zaidi zinasema kuwa Awale alisimamamishwa na askari, ambao walimchukua kwenye gari lao huku wakilitelekeza gari lake kwenye maeneo hayo.
 
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, aliliambia Nipashe atalizungumzia suala hilo leo pamoja na mambo mengine.

Jeshi la polisi linamshikilia mwanamkakati wa timu ya kampeni ya aliyekuwa mgombea urais wa Chadema
“Nimewaagiza vijana wangu waniandalie taarifa juu ya suala hilo. Nitalizungumzia jambo hilo kesho (leo) pamoja na mambo na mengine,” alieleza Kamishna Kova, ambaye hakutaka kuingia kwa undani wakati alipohojiwa na gazeti hili kuhusiana na suala hilo.
 
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kwamba kukamatwa kwa Awale kunahusishwa na masuala ya Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni kutokana na ukaribu wake na Lowassa.
 
Lowassa alishindwa kwenye uchaguzi wa urais baada ya kushika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072, 848 sawa na asilimia 39.97 wakati mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.
 
Awale alikuwa miongoni mwa viongozi waandamizi kwenye timu ya kampeni ya Lowassa tangu wakati alipokuwa mwanachama wa CCM.
 
Lowassa alipoachana na CCM na kujiunga na Chadema, Julai 28 mwaka huu, Awale alikuwa miongoni mwa watu waliofuatana naye.
 
Awale alikuwa miongoni mwa watu waliofuatana Lowassa siku anatambulishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, baada ya kujiunga rasmi na chama hicho.
 
Kabla ya kuingia kwenye masuala ya siasa, Awale alikuwa Ofisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Stanbic nchini Tanzania kabla ya kuachia ngazi mwaka 2013.
 
Aliiongoza benki ya Stanbic kuanzia mwaka 2006, lakini kabla ya hapo alikuwa akifanya kazi katika Benki ya Citibank.
Tangu alipoachana na Stanbic, Awale alikuwa miongoni mwa wanamkakati waandamizi wa Lowassa tangu alipokuwa akiwania kugombea urais kwa tiketi ya CCM.
 
Lowassa alipokatwa jina lake CCM na kujiunga na Chadema, Awale alikuwamo kwenye timu ya kampeni akiwa miongoni mwa viongozi waandamizi.
 
Pamoja na kuwemo kwenye timu ya kampeni, pia ni anachukuliwa kama miongoni mwa wasaidizi na washauri muhimu wa Lowassa.
 
Kukamatwa kwa Awale kunakuja baada ya hivi karibuni vijana wanane waliokuwa wakisaidia kazi ya kujumlisha kura za Lowassa kwenye kituo cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujumlisha matokeo ya kura za urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 NIPASHE