Breaking News

Jumamosi, 2 Januari 2016

Dk Makongoro amponda Dk Magufuli




MAGUFULI HAKUPUNGUZA UKUBWA WA SERIKALI AMEONGEZA.
Na Dr. Milton Makongoro Mahanga
Kwa kuteua makatibu wakuu 27 kiuhalisia rais magufuli kaunda serikali yenye wizara 27 huku akituaminisha kwamba ni wizara 19. Hivyo siyo kweli kwamba kapunguza ukubwa wa serikali bali kaongeza ukubwa wa serikali.
Sina hakika kama wasaidizi wa rais wamemshauri na kumweleza kwamba wizara si ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya katibu mkuu (mtendaji mkuu, afisa masuhuli). Mtendaji mkuu ndiye mwenye dhamana. Ndiyo maana hata katika ngazi ya kata, ofisi ile inaitwa Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata siyo ofisi ya Diwani.
Kwa hiyo magufuli alipounda, kwa mfano, wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi (ambazo zilikuwa wizara mbili kabla) na kuteua makatibu wakuu (maafisa masuhuli) watatu kiuhalisia hakuunganisha wizara mbili kuwa moja bali ameunda wizara tatu kutoka mbili za awali. Ameongeza ukubwa wa serikali.
Kwa hiyo anazoita wizara tano za (1) bunge, uratibu, kazi, ajira na walemavu; (2) kilimo, mifugo, na uvuvi; (3) ujenzi, uchukuzi na mawasiliano; (4) viwanda, biashara na uwekezaji; (5) Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, na akateua makatibu wakuu 13 kwenye wizara hizo 5, kiuhalisia ameunda wizara 13 hapo ambazo kabla ya hapo zilikuwa wizara 11.
Lazima ieleweke kwamba ukubwa wa serikali hautegemei sana wingi wa mawaziri bali wingi wa makatibu wakuu. Nitaeleza kwa kutoa mfano wa gharama. Ongezeko la gharama kwa kuongeza waziri mmoja ni ndogo sana kulinganisha na kuongeza katibu mkuu mmoja. Waziri anapoteuliwa tayari anakuwa ni mbunge mwenye mshahara wake wa ubunge na kinachoongezeka ni kama laki 5 tu juu ya ule mshahara wa ubunge na gharama zingine ndogo za gari n.k., na pia mishahara na gharama za katibu muhtasi, msaidizi na dereva. Lakini katibu mkuu anaingia upya na mshahara kamili na gharama zingine nyingi na wasaidizi. Aidha kwa mfano wa wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi kwenye makatibu wakuu watatu lazima kila katibu mkuu atakuwa na idara na wakurugenzi kadhaa. Kama kwa mfano kitengo cha uvuvi kilikuwa na idara moja au mbili katibu mkuu mpya wa uvuvi atataka kuongeza idara na wakurugenzi zaidi. Hizo ni gharama za ziada kwa serikali..
Kumbuka katibu mkuu awe na naibu au hapana si hoja, hoja ni kwamba atakuwa na idara kadhaa zenye wakurugenzi (wanaotakiwa kuwa wataalam wa fani za idara yao). Kwa mfano bila kujali ukubwa wa wizara, kwa mfano, ya kilimo, ufugaji na uvuvi, rais magufuli angeteua katibu mkuu mmoja (na naibu wake) halafu akateua wakurugenzi wazuri ambao ni wataalamu kila mmoja kwenye idara za kilimo, ufugaji na uvuvi. Sasa ukiwa na wakurugenzi kama hao makatibu wakuu kila kitengo wa nini? Labda rais magufuli atuambie kwamba hatateua tena wakurugenzi wa kilimo, wa mifugo na wa uvuvi, na kwamba hao makatibu wakuu wa vitengo hivyo watatosha. Lakini hili haliwezekani.
Ukiacha hayo ya msingi sasa angalia hii mpya aliyofanya rais magufuli kwenye wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji. Ameteua naibu katibu mkuu mmoja kuwa chini ya makatibu wakuu wawili! Kwa tuliosoma "chain of command" kwenye "management" tunajua kwamba kila mtumishi lazima awe na "immediate boss" mmoja tu. Sasa huyu naibu katibu mkuu bosi wake hasa atakuwa katibu mkuu wa viwanda au katibu mkuu wa biashara na uwekezaji? Na je mabosi hawa wawili wote wakimpa kazi kwa wakati mmoja ataanza na kazi ya yupi? Na je yule ambaye kazi yake itacheleweshwa (kwa sababu naibu katibu mkuu kaanza na kazi ya katibu mkuu mwingine) atajisikiaje au atachukua hatua gani katika enzi hizi za hapa kazi tu? Au itabidi makatibu wakuu hawa wawili washauriane kwanza kabla ya kumpa majukumu naibu katibu mkuu wao?
Kwa ujumla ahadi ya magufuli kwenye kampeni kwamba ataunda serikali ndogo hakuitimiza. Ameongeza ukubwa wa serikali. Rais magufuli atambue kwamba udogo wa baraza la mawaziri kamwe si udogo wa serikali.
Dr. Milton Makongoro Mahanga

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni