Mmoja wa Majenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walioteuliwa kushika nyadhifa nyeti serikalini,Meja Jenerali Gaudence Milanzi,ameanza kazi kwa kutoa tahadhari kwa majangili akisema atatumia mbinu za medani kuwakabili na kuwatokomeza kabisa.
Akizungumza Muda mfupi baada ya kuapishwa mbele ya Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu Wizara Ya Mali Asili na Utalii,Meja Jenerali Milanzi alisema ni aibu Tanzania kuendelea kupoteza wanyama pori bila hatua stahiki kuchukuliwa.
"Siwezi kuvumilia kuona serikali ikishindwa kusimamia rasilimali za nchi ambazo ndizo zinaoongeza idadi ya watalii nchini na pato la taifa.Majangili wanaongozwa na uchu na uchoyo kwa watanzania wengine.
"Maliasili zilizopo ni kwa ajili ya kuwanufaisha watanzania wote na kuliletea sifa taifa letu.Ni aibu kuonyesha dalili za kushindwa katika mapambano dhidi ya ujangili.Maliasili na utalii ndio kitovu cha mapato ya taifa, kwani wanyama hasa wale adimu ndio huvutia watalii.
"Nitatumia mbinu na uwezo wangu wa kijeshi kukabiliana na hilo,kwa sasa ni mapema kusema lolote.Kuna mambo mengi ninatakiwa nijifunze kwanza,lakini tutaangazia matatizo yote yanayoikabili wizara hii nyeti.
"Kuna masuala ya vitalu vya uwindaji,kuna tatizo la wananchi kuwepo ndani ya hifadhi za taifa;yote tutayaangazia pamoja na kuangalia namna ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhifadhi na ujangili." Alisema Meja Jenerali Milanzi.
Kwa upande mwingine,Katibu mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi,Jaji Meja Jenerali Projest Rwegasira, alisema kwanza atahitaji muda kujua sheria na taratibu za jeshi la Polisi ili asichanganye mambo katika utendaji wake.
Wiki iliyopita,Rais Magufuli aliwashangaza watu alipowateua maofisa hawa wa juu wa JWTZ kuziongoza wizara hizo nyeti, kitendo ambacho hakijazoeleka sana.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence S.Milanzi akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika jana katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Jaji Meja Jenerali Projest A.Rwegasira akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam. Source Tuangaze
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni