Breaking News

Jumamosi, 2 Januari 2016

Kamanda Kova astaafu rasmi Jeshi la Polisi


Aliyekuwa kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova amestaafu huku akisema, katika kipindi alicholitumikia jeshi hilo, hatasahau matukio matatu maishani mwake.
Kova amestaafu baada ya kuongoza kanda hiyo tangu Juni 2008.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti vya utumishi bora askari na raia waliotoa ushirikiano kwa polisi, kwenye viwanja vya Chuo cha Maofisa wa Polisi Kurasini, Kova ambaye kabla, alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, alisema uchapakazi wake haukuanzia huko kwani kabla ya hapo alikuwa Kigoma ambako aliongoza vita ya kuzagaa kwa silaha miongoni mwa raia.
“Ingawa sipendi kukumbuka historia hii, nilifanya kazi kubwa kule ambayo ilichangia wakubwa kuona nafaa kuja kutumika kwenye jiji hili, ambalo ni kubwa kuliko yote nchini,” alisema Kova aliyestaafu rasmi baada ya kufikisha umri wa kisheria ikiwa ni pamoja na kuongezewa mkataba na mamlaka ya uteuzi.

Matukio
Katika hafla hiyo aliyotumia kutangaza kuwa anamwachia mikoba yote Simon Siro kuwa kaimu kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Kova alitaja matukio yanayoacha kumbukumbu kichwani mwake kuwa ni: kwanza, uvamizi uliofanywa na majambazi katika Kituo cha Polisi Stakishari; pili, kuanguka na helikopta aliyokuwamo pamoja na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi (sasa Rais), Dk John Magufuli. Tukio la tatu ni mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita.
“Muda wangu umekwisha. Nimelitumikia Jeshi la Polisi kwa zaidi ya miaka 40. Haikuwa kazi rahisi kama watu wanavyodhani. Ila namshukuru Mungu kwani sikuifanya kazi pekee yangu,” alisema.
“Kabla sijaondoka nilimuuliza IGP Ernest Mangu kama nina kosa, akanijibu sina. Ndiyo maana leo (jana), nikiwa sina kinyongo, nakabidhi kijiti hiki kwa Simon Siro,” alisema Kamishna Kova huku akimshika mkono Kamanda Siro.
Alimtaka Siro kuendeleza mazuri alioyaacha ili afanye kazi zake kwa ufanisi, lakini pia alimtaka asiwe mpole kazini na asisahau kuendelea kudai masilahi ya askari zikiwamo nyumba.
Kwa upande wake, Kamanda Siro alisema: “Natoa onyo kwa vijana wanaofanya uhalifu hasa wa kutumia pikipiki. Nitakula nao sahani moja, nikishirikiana na walinzi shirikishi kwani wahalifu hawa ni wachache sana,” alisema Siro.

Kujitosa siasa
Baada ya kupata uzoefu wa kutosha zinavyoendeshwa harakati za kisiasa kuanzia mwaka 2010 na mwaka jana, Kova amesema upo uwezekano wa yeye kujitosa kwenye siasa.
“Msinishangae siku moja nitakapojiunga na chama chochote cha siasa. Nimestaafu kulitumikia jeshi na huu ni mwanzo wa mambo mengine. Masuala yangu binafsi yanaanzia hapa,” alisema. Mbali ya siasa alisema anaweza kufanya kazi nyingine yoyote. “Naweza nikaajiriwa mahali popote na nikawajibika kama inavyotakiwa,” alisema Kova ambaye awali, alikuwa anabanwa na sheria ya utumishi wa umma kujihusisha na vyama vya siasa.

Mahita
Omary Mahita, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi enzi za utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, alimpongeza Kova kwa kazi njema aliyoifanya: “Amefanya kazi nzuri. Alishirikiana vizuri na wenzake kama inavyotakiwa na hilo limemwongezea mafanikio.”

CHANZO: MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni