Breaking News

Jumatatu, 14 Desemba 2015

Sumaye,Lowassa,Kingunge ni Chatu mbele ya Mbwa

Na Thadei Ole Mushi.
Nilishawahi kukaa na wawindaji walinihadithia hadithi moja kuwa Mbwa hujipeleka kwa chatu mwenyewe angali akijua anaenda kumezwa. Wawindaji hawa waliniambia kuwa Chatu amuonapo Mmbwa hutoa harufu moja ambayo mbwa huipenda kweli na mbwa humfuata Chatu mwenyewe na kumezwa. Wakati mbwa akimfuata chatu huenda akilia kwani anajua kinachoenda kumkuta mbeleni.
Kisa hiki nimekikumbuka ninavyona Chadema kinavyowapokea kina Sumaye. Najua wanajua madhara ya kuwapokea watu wenye makando kando ila kuna harufu watu hawa wanaitoa na inawavutia kina Mbowe. Hivyo wanawapokea ila najua Moyoni mwao kuna manunguniko makuu.
Ili hili Taifa liendelee kwa kasi linahitaji pia upinzani wenye tija na upinzani wenye nguvu. Sijui kama nyie wenzangu mnaona haya ninayoyaona mimi kuhusu chama cha CHADEMA , ambacho kimeendelea kukipa changamoto chama changu na kukifanya kufanya kazi na usiku. Naamini pia bila CHADEMA hakuna pia CCM imara, CHADEMA wanafanya kazi ya (watch dog) kila mtu akipotoka ndani ya serikali CHADEMA kinapaza sauti na Kumrudisha kwenye mstari. Ndio Maana nahitaji pia CHADEMA kikue na kiwe na uwezo hata wa Kuchua dola ili kiwe mbadala wa CCM baadaye.
Jana nimesikia aliyekuwa waziri mkuu mstaafu kahamia Chadema na kupewa kadi ya chama na mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe. Mimi sina tatizo na Chadema kupata wanachama wapya ila nina tatizo na aina ya wanachama wenyewe wanaohamia kwa sasa.
Tumeona faida na hasara za Lowassa kuhamia chadema, ni kweli kuwa Lowassa amekisaidia chama kwa upande mmoja kuongeza wabunge na hata ruzuku najua itaongezeka. Wakati unahesabu faida ya ujio wa Lowassa pia uhesabu na hasara yake kuhamia ndani ya Chadema.
Ni ukweli kwamba Chadema kwa sasa kimekosa hoja ya kujinasibu nayo kisiasa. Kama nilivyowahi kusema agenda ya UFISADI ilikuwa ndio agenda iliyokikuza chama hicho ila kwa sasa hawana tena hoja hiyo kutokana na waliowatukana na wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndio wanakiongoza chama.
SUMAYE, LOWASSA NA KINGUNGE UGONJWA UTAKAOKIFUTA CHADEMA KABISA KWENYE RAMANI ZA SIASA.
Hawa kwa pamoja ni wanasiasa wanaounganishwa na agenda moja tu yenye malsahi kwao nayo ni "URAISI" ukiondoa agenda ya uraisi miongoni mwa watu hawa ni maadui wa kutupwa. Maslahi ndio yanayowaunganisha na sio itikadi za chama au hawakujiunga CHADEMA kwa kuwa wanavutiwa na sera za CHADEMA la Hasha!!!.
Sumaye ameamua rasmi kuhamia jana Chadema kwa kuwa ameona uchochoro wa kutimiza ndoto zake za kuwa raisi wa nchi hii baadaye.
Sumaye anajua fika kuwa baada ya miaka 5 Lowassa hatakuwa na nguvu aliyonanyo hivyo chama kitampa nafasi ya kugombea. Hili ni hatari kama Lowassa ataendelea kuimarika kiafya kama nilivyomuona kwenye msiba wa Mawazo. Kama hali ya Lowassa itaendelea hivi hatakubali kunyanganywa nafasi ya kugombea na tukumbuke kuwa Lowassa nje ya chadema ni taasisi inyaojitegemea chini ya 4U Movement.
Kitakachotokea kuanzia sasa ni Lowassa na Sumaye kuendelea kujijenga kila mmoja kwa style yake huku jicho na fikra za kila mmoja wao zikilenga 2020 na sio kukisaidia Chama kujijenga kama Taasisi, baadaye kwenye mchakato wa kumpata mtu wa kukiwakilisha chama kwenye nafasi ya uraisi kila mmoja atataka awe yeye na watapasuka na chama kitakosa mwelekeo. Kama watu hawa hawatadhibitiwa sijui kama chama kitaweza kuhimili mpasuko wake baadaye.
Watu hawa pia wanazuia watu wenye vipaji vya uongozi na wenye uwezo zaidi ndani ya Chadema kupata nafasi ya kugombea Uraisi. Hata aje Malaika ndani ya chadema akataka kugombea Uraisi mbele ya Sumaye na Lowassa hawatapewa nafasi. Pia wanazuia watu wasafi kujiunga na Chadema kwani watahesabiwa kuwa fungu moja la wachafu. Ni aibu kwa chama kama chadema leo kuogopa kuukemea ufisadi.
CHADEMA wanapaswa kufungua macho hapa na kuwadhibiti watu hawa. Aidha makandokando yao yatakichafua pia chama ni bora Sumaye angehamia NCCR kwa kuwa kipo ndani ya Ukawa mchango wake bado ungeonekana. Chukua makando kando ya sumaye changanya na ya Lowassa halafu usisahau agenda waliyoibeba kichani sioni CHADEMA ikipona.
Tuvute subira wale vijana wasiotaka kufikiri ni ruksa kutukana kwani ndio malezi wanayopata huko waliko.
OLE Mushi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni