Breaking News

Jumatatu, 7 Desemba 2015

Mbona Wakenya wanamkaribisha Kenyatta kama mgeni?

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amefanya ziara 43 nje ya nchi tangu kuingia madarakani miaka mitatu iliyopita na Alhamisi wiki hii anatarajiwa kuzuru Kigali, Rwanda.
Ziara hizi zimeonekana kuwakera wananchi wengi ambao wameingia kwenye mitandao ya kijamii kuzikosoa.
Kwa takriban siku mbili, jumbe za kukejeli safari hizo zimekuwa mada kuu katika mitandao ya kijamii, Wakenya wakitumia kitambulisha mada #UhuruInKenya.
Wanalinganisha kurejea kwa Rais Kenyatta nchini Kenya kutoka Afrika Kusini na ziara zilizofanywa na viongozi mashuhuri duniani kama vile Rais Barack Obama mwezi Julai na Papa Francis mwezi Novemba. Vitambulisha mada vilivyotumiwa wakati huo vilikuwa #ObamaInKenya na #PopeInKenya.
Bw Kenyatta amefanya ziara 43 katika muda ambao amekuwa uongozini, ambazo zinazidi ziara 33 za nje ya nchi alizofanya mtangulizi wake Rais mstaafu Mwai Kibaki miaka kumi aliyokuwa mamlakani.
Ziara hizo za Rais Kenyatta zinakadiriwa kugharimu Sh2.1 bilioni, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation.
Lakini ikulu imetetea ziara hizo ikisema zimeletea Kenya manufaa tele.
Msemaji wa Rais Manoah Esipisu alihutubia wanahabari Jumapili na kusema Bw Kenyatta amefanikiwa kupata ufadhili wa miradi ya miundo mbinu, elimu, kawi na masoko ya bidhaa.
Kunao wanaoamini ziara hizo zinastahiki, kwa mfano mdadisi wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi anayesema Bw Kenyatta anafaa kuachwa afanye kazi.
Baadhi ya Wakenya wamelinganisha mtindo wa Bw Kenyatta na kiongozi wa taifa jirani la Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ambaye kwa mwezi mmoja ambao amekuwa madarakani ameonekana kutilia mkazo sana kupunguzwa kwa matumizi ya fedha za umma.
Amefuta ziara nyingi za ng'ambo na kuwapa mabalozi wa taifa hilo nchi za kigeni jukumu la kuwakilisha taifa.
Dkt Magufuli ametumia kauli mbiu ya "Hapa Kazi Tu" wakayi wa kampeni na baada ya kuingia uongozini. Kauli mbiu hii imefanyiwa ukarabati na baadhi ya watu na kugeuzwa kuwa "Hepa Kazi" upande wa kiongozi wa Kenya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni